Na Mwandishi wetu
Clatous Chama ameibuka shujaa baada ya kufunga bao la kusawazisha lililoiwezesha Simba kutoka sare ya bao 1-1 na Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Ijumaa hii, Azam ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 14 mfungaji akiwa Prince Dube.
Bao hilo lilidumu kwa kipindi chote cha kwanza na licha ya Simba kupambana kutaka kusawazisha lakini juhudi zao ziligomba mwamba mbele ya ukuta wa Azam.
Chama ambaye klabu yake ilimsimamisha hivi karibuni kwa kilichodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu kabla ya kumsamehe, alisawazisha bao hilo katika dakika tatu za nyongeza akitumia vizuri mpira wa adhabu.
Bao hilo lilipokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Simba ambao waliingiwa na hofu ya timu yao kupoteza mchezo ingawa pia walishindwa kuzitumia nafasi kadhaa walizotengeneza ambazo zingeweza kuwafanya watoke na pointi zote tatu.
Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati Azam inabaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 32 katika mechi 14.
Yanga ambayo inasubiri kuumana na Prisons kesho Jumapili hadi sasa ndiyo inayoshika usukani wa ligi hiyo ikiwa imejikusanyia pointi 37 katika michezo 14.
