Abidjan, Ivory Coast
Kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Hugo Broos bado (pichani) hajakubaliana na ukweli kwamba timu yake imetolewa katika Afcon 2023, badala yake anaamini timu hiyo ilicheza vizuri na ilitakiwa kushinda mechi hiyo.
Afrika Kusini au Bafana Bafana ililala kwa penalti 4-2 mbele ya Nigeria jana Jumatano usiku baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi ya nusu fainali ya Afcon.
Bafana Bafana ilipambana vizuri na kufanikiwa kusawazisha bao kwa mkwaju wa penalti katika dakika za lala salama lakini mambo yakawa magumu kwao kwenye mikwaju ya penalti.
“Soka kuna wakati ni mchezo mgumu, unapoangalia kiwango cha uchezaji cha timu yangu hii leo (jana) na baada ya hapo zinakuja penalti na unajikuta ukipoteza na haupo kwenye fainali, ni ngumu kukubali kwa sababu tulicheza vizuri,” alisema Broos.
“Nafikiri tulikuwa timu bora nusu ya kwanza, tulipata nafasi nzuri, Nigeria hawakuwa na nafasi yoyote, kipindi cha pili walipata nafasi chache zilizowapa goli na tulibadili kitu kwenye mbinu na kurudi vizuri,” alisema Broos.
Broos alisema kwamba timu yake ilitengeneza nafasi nyingi na hiyo maana yake ni kwamba kama wangefunga wao ndio wangekuwa fainali na si Nigeria.
Kocha huyo kutoka Ubelgiji hata hivyo aliipongeza timu yake kwa kucheza vizuri fainali za Afcon tangu mwanzo hadi kwenye mechi ya nusu fainali walipokwamia.
“Ni pigo kubwa kwa kila mmoja, tunaamini tulikuwa na mchezo mzuri, si leo tu lakini ni kwa kipindi chote cha fainali hizi, najivunia wachezaji wangu, maumivu yapo lakini kuna kitu cha kujivunia,” alisema Broos.
Baada ya matokeo hayo, Bafana Bafana sasa inasubiri kuumana na DR Congo keshokutwa Jumamosi katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu.
