Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ameibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari wa klabu hiyo inayodhaminiwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Mzize ametwaa tuzo hiyo akiwashinda wachezaji wenzake, Gift Fredy na Willson Chigombo kutoka kikosi cha vijana ambaye alifanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika Zanzibar hivi karibuni.
Akizungumza baada ya kushinda tuzo hiyo inayotokana na kupigiwa kura na mashabiki wa timu hiyo, Mzize aliwashukuru wote waliompigia kura na kueleza kuwa tuzo hiyo imemuongezea ari ya kujituma zaidi ili kuingia tena kwenye kinyang’anyiro siku zijazo.
“Nawapongeza mashabiki wa Yanga, kwa kunipigia kura maana tuzo hii imeniongezea ari ya kuzidi kujituma kuisaidia timu yangu lakini na mafanikio yangu binafsi,” alisema Mzize.
Baada ya kuibuka mshindi mshambuliaji huyo anatarajiwa kupewa kitita cha Sh 4,000,000, pamoja na kombe dogo.
Mbali na Mzize wachezaji wengine wa Yanga ambao wamewahi kushinda tuzo hiyo ni Stephane Aziz Ki (Oktoba), Pacome Zouzoua (Novemba) na Djigui Diarra aliyeibuka mshindi wa Desemba.
Wakati huo huo, taarifa za ndani kutoka Yanga zinaeleza kuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Diarra alitarajiwa kujiunga na wenzake jioni ya Jumatano akitokea kwao Mali alikokwenda kuitumikia timu yake ya taifa iliyokuwa ikishiriki michuano ya Afcon inayoendea nchini Ivory Coast.