Abidjan, Ivory Coast
Matumaini ya baadhi ya Watanzania kuiona DR Congo ikicheza mechi ya fainali ya Afcon 2023 yamekwama baada ya timu hiyo kulala kwa bao 1-0 mbele ya wenyeji Ivory Coast ambao ndio watakaocheza mechi ya fainali dhidi ya Nigeria.
Mshambuliaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Sebastien Haller ndiye aliyefuta ndoto za DR Congo baada ya kupachika bao pekee la ushindi kwa Ivory Coast katika dakika ya 65 ya mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo Alhamisi.
Haller alifunga bao hilo kwa shuti kali akiitumia vizuri pasi ya Gradel na kupiga mpira uliomshinda kipa wa DR Congo, Lionel Mpasi na kuifanya DR Congo ishindwe kuiweka rekodi iliyokuwa ikisubiriwa na wengi.
Ushindi huo unakuwa jambo kubwa kwa wenyeji Ivory Coast ambao walilazimika kumtimua kocha wao, Jean-Louis Gasset na nafasi yake kukabidhiwa kocha wa muda, Emerse Fae ambaye hatimaye ameifikisha timu hiyo hatua ya fainali.
Fae, 40, kiungo wa zamani wa timu za Nantes na Nice za Ufaransa na Reading ya England, sasa ana mtihani mmoja wa kuiwezesha Ivory Coast kubeba taji la tatu la Afcon katika mechi ya fainali itakayopigwa Jumapili ijayo.

Ivory Coast, timu mwenyeji iliyozianza fainali za Afcon 2023 kwa kusuasua hatimaye imewapa faraja mashabiki wake ambao wanaisubiri kwa hamu Jumapili wakiamini timu yao inaweza kulibeba taji hilo baada ya kufanya hivyo mwaka 1992 na 2015.
Katika hatua nyingine wachezaji wa DR Congo na kocha wao, Sebastien Desabre walifanya mgomo wakati wa kuimba nyimbo za taifa kwa kuziba midomo wakitaka amani itafutwe mashariki mwa nchi yao.
Mechi nyingine ya nusu fainali iliyochezwa mapema jana Jumatano, Nigeria au Super Eagles ilifanikiwa kuitoa Afrika Kusini au Bafana Bafana kwa penalti 4-2 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Nigeria ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na William Troost-Ekong kwa mkwaju wa penalti baada ya Victor Osimhen kuchezewa rafu ndani ya eneo la penalti na beki wa Bafana Bafana, Mothobi Mvala.
Bafana Bafana walifanikiwa kusawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penalt ya dakika ya 90 iliyofungwa na Teboho Mokoena na kuizuia Nigeria kwenda fainali moja kwa moja hadi sheria ya penalti tano tano ilipotumika na Nigeria kuibuka kinara.
