Na mwandishi wetu
Taasisi ya Fountain Gate Sports Academy imeingia mkataba wa miaka miwili na mtaalamu wa ufundi, Frank Petersen, lengo ni kuwatafutia timu wachezaji kwenda kucheza mpira nje ya Tanzania.
Mkataba huo umesainiwa leo Jumatatu mjini Dodoma ambao pia una kipengele cha kuongeza muda zaidi baada ya kumalizika huu wa sasa.
Akizungumza baada ya kukamilisha zoezi la kusaini mkataba huo, Petersen aliyewahi kufanya kazi hiyo nchi za Msumbiji, Uganda na Nigeria amesema ifikapo Julai mwaka huu baadhi ya wachezaji watakwenda Denmark kufanya majaribio na wengine kusajiliwa kabisa.
“Nimevutiwa na namna ambavyo Fountain Gate Sports Academy imetengeneza utaratibu mzuri zaidi kwenye akademi yao tofauti na nchi nyingine zote ambazo nimepita, nafurahi kufanya nao kazi,” alisema Petersen.
Petersen ameongeza kuwa kitu kingine kilichomvutia zaidi ni misingi yao ya soka kwa kuwa ameona kuna watoto hadi wa mwaka mmoja wanafanya program nyingi za michezo hasa mpira wa miguu.
Naye Mkurugenzi wa Fountain, Japhet Makau alisema: “Mkataba huu ni wa miaka miwili lakini utakuwa unapitiwa kila baada ya miezi sita kujiridhisha kama tunapata kile tunachostahili. Ushirikiano huu si michezo tu hata shuleni pia tutanufaika kuwawezesha vijana kupata nafasi zaidi Denmark.”
