Abidjan, Ivory Coast
Kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui amesema anabeba lawama zote za timu hiyo kutolewa kwenye fainali za Afcon hatua ya 16 bora baada ya kufungwa mabao 2-0 na Afrika Kusini.
Morocco au Atlas Lion ilishindwa kutamba juzi Jumanne mbele ya Afrika Kusini na kutolewa kimaajabu jambo lililowashangaza wengi kwa kuwa ni moja ya timu zilizopewa nafasi ya kubeba taji hilo.
Timu hiyo ilianza kwa kuadhibiwa kwa bao la Evidence Makgopa dakika takriban 10 baada ya kuanza kipindi cha pili kabla ya Teboho Mokoena kumalizia bao la pili katika dakika za lala salama.
Morocco mbali na nyota wake, Achraf Hakimi kukosa penalti lakini pia ilimaliza mechi na wachezaji 10 baada ya kiungo wake, Sofyan Amrabat kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
“Labda tungeweza kumaliza mechi katika nusu ya kwanza, lakini katika hatua tuliyofikia unaweza kuadhibiwa kwa nafasi yoyote unayoipoteza,” alisema Regragui.
“Penalti umetuuma sana na hakika hatukufanya kila kitu tulichotakiwa kukifanya lakini mimi nabeba lawama zote,’ alisema Regragui.
Matumaini ya Morocco yalikuwa ni kubeba taji la Afcon kwa mara ya kwanza tangu ifanye hivyo mwaka 1976 na mafanikio yao ya kufikia nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 yalifanya matumaini ya kubeba taji hilo kuwa makubwa zaidi.
“Tutajifunza kutokana na mkwamo huu ambao hatukuutarajia, hili ni jambo la kuumiza kwa mashabiki wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono kwa kiasi kikubwa,” alisema Regragui.
