Na mwandishi wetu
Timu ya Geita Gold imesema akili yake yote kwa sasa imeelekea katika mchezo ujao wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Simba utakaochezwa Februari 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Samwel Dida ambaye ni Ofisa Habari wa Geita amesema leo Jumatano kuwa baada ya kuona ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu, mchezo ulioko mbele yao ni dhidi ya Simba ambao wanafahamu ugumu wake, hivyo wanafanya maandalizi ya kurejea mapema Mwanza kujipanga.
“Ratiba inaonesha tuna mchezo Februari 12, bado tupo kambini Morogoro tunafanya maandalizi ya mwisho turudi Mwanza kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba ambao huenda ukawa mgumu kulingana na ubora wa wapinzani, tunahitaji kuwa imara zaidi,” alisema.
Alisema malengo waliyoweka kuelekea lala salama ya ligi kuu ni kufanya vizuri katika michezo yote iliyobaki na hilo lazima litimie kwa sababu wana kikosi kizuri na wameshafanya marekebisho chini ya kocha wao mpya, Denis Kitambi.
“Tuwatoe hofu mashabiki zetu, tutafanya vizuri, maandalizi yanatupa mwelekeo, hakuna tunachokihofia,” alisema.
Kwenye msimamo wa ligi, unaonesha Geita iko katika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza michezo 13, kushinda minne, sare nne na kupoteza mitano.
