Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza (pichani) amesema hata kama ligi ikianza leo, kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu NBC.
Akizungumza na GreenSports leo Ijumaa, Baraza alisema imani hiyo inatokana na maandalizi waliyoyafanya kipindi hiki ambacho ligi imesimama kupisha michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) inayoendelea nchini Ivory Coast.
“Tupo tayari kwa vita ya pointi tatu, tumepata muda wa kutosha kurekebisha mapungufu yetu lakini pia tumecheza mechi kadhaa za kirafiki ambazo zimetuimarisha na kujiona tupo tayari kwa kazi,” alisema Baraza.
Kocha huyo raia wa Kenya, alisema anajua wanakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba, lakini wamejipanga kuhakikisha wanachukua pointi zote tatu kwenye mchezo huo ambao utachezwa kwenye uwanja wao wa Jamhuri, Dodoma.
Dodoma Jiji inashikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 18 katika michezo 13 waliyocheza hadi sasa.