Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Geita Gold, Denis Kitambi ameanza kukisuka upya kikosi chake kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu NBC.
Kitambi aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni amesema leo Jumatano kuwa baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Fountain Gate ameona mapungufu kadhaa, anahitaji kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa ligi mwezi ujao.
Geita Gold imeweka kambi mkoani Morogoro kwa ajili ya kujiandaa na ligi na mashindano ya Kombe la Shirikisho la FA (ASFC).
“Katika wiki mbili za kambi yetu tumejaribu kuangalia utimamu wa mwili, naridhishwa na maendeleo, kikubwa tunachohitaji kufanyia kazi ni kujenga mashambulizi kuanzia nyuma kwa sababu tunahitaji muunganiko wa timu kuanzja nyuma na kuanzia wiki ijayo nitafanyia kazi hilo,”alisema Kitambi.
Alisema hata wachezaji wapya waliowasajili hivi karibuni wamekuwa na muunganiko na maelewano mazuri juu ya mfumo wake anaouandaa kwa timu hiyo, hivyo hiyo inampa morali ya kuendelea kuijenga vyema timu hiyo.
