Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Yanga umeanza mchakato wa kutafuta timu za nje zitakazocheza mechi ya kirafiki na kikosi chao kipindi hiki cha maandalizi kabla ya mwendelezo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha mkuu wa miamba hiyo, Miguel Gamondi ameeleza leo Jumatatu kuwa amezungumza na uongozi wa timu hiyo kumtafutia mechi mbili za kirafiki za kimataifa ili kujua uimara wa kikosi chake kabla ya mechi mbili za mwisho za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alisema wameanza jitihada za kutafuta timu hizo na anaamini mchakato huo hautochukua muda kukamilika sababu wana maelewano mazuri na timu nyingi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Lengo letu ni kupata timu imara ambazo zitakipa kikosi chetu mazoezi mazuri kulingana na mashindano tuliyopo, ndio maana nikasema mchakato wa kuzisaka timu hizo umeanza na dhamira yetu ni kucheza mechi hizo tukiwa ugenini,” alisema Arafat.
Kikosi cha Yanga kimerejea kambini Avic Town wiki mbili zilizopita kujiandaa na Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu NBC na Kombe la ASFC huku timu hiyo ikiwakosa baadhi ya nyota wao waliopo kwenye timu zao za taifa zinazoshiriki michuano ya Afcon nchini Ivory Coast.
