Na mwandishi wetu
Bondia Hassan Mwakinyo amesema maandalizi ya pambano lake dhidi ya Mbiya Kanku raia wa DR Congo yamekamilika, mashabiki wake wasubiri kushuhudia burudani ya ngumi.
Pambano hilo la kuwania mkanda wa WBO Afrika, litakuwa la raundi 10 ambalo litafanyika Januari 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex mjini Unguja, Zanzibar.
“Najua naenda kukutana na bondia mzuri lakini mimi ni bora kuliko yeye, nipo tayari kwa ajili ya kupanda ulingoni nataka kulitumia pambano hili kuonyesha urejeo wangu,” aliseme Mwakinyo.
Mwakinyo, bondia mwenye hadhi ya nyota mbili na nusu amecheza michezo 24 akishinda mapambano 21 kwa KO huku akipoteza mapambano matatu, mawili kati ya hayo akipigwa kwa KO.
Kanku bondia mwenye hadhi ya nyota moja na nusu amecheza mapambano 18 akishinda 11 yote kwa KO, amepata sare moja huku akiwa amepoteza sita, matano kati ya hayo akipigwa KO.
Hili litakuwa ni pambano la kwanza kwa Mwakinyo tangu lilipotokea sakata lake la kugoma kupanda ulingoni Septemba mwaka jana kwa ajili ya kuzichapa na Julius Indongo na kisha kufungiwa na baadae kufunguliwa mwezi uliopita na TPBRC.