Na mwandishi wetu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya taifa, Taifa Stars kwa mchezo mzuri waliouonesha walipokipiga na Morocco kwenye michuano ya Afcon licha a kufungwa mabao 3-0.
“Mchezo mzuri usiku wa leo (jana), vijana wetu Taifa Stars japo bahati haikuwa upande wetu,” aliandika katika salamu zake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X zamani Twitter.
Rais Samia pia aliitakia heri timu hiyo na kusema taifa liko nyuma yao katika mechi zinazofuata baada ya jana Jumatano kupoteza kwa Morocco kwenye Uwanja wa Laurent Palou, San Depro nchini Ivory Coast.
Akieleza kuhusu kupoteza mchezo huo, kocha mkuu wa Stars, Adel Amrouche amefafanua kuwa mpango wake ulishindwa kufanya kazi ndio maana walifungwa mabao matatu.
“Mpango wetu wa mchezo ulishindwa. Hatukutarajia hali hii, lakini ninawapongeza Morocco kwa mchezo mzuri pamoja na matokeo mazuri.
“Ubora wa wachezaji wa Morocco ulionesha utofauti na walistahili kushinda ingawa tulitaka matokeo mazuri lakini pia tulifanya makosa binafsi,” alielezea Amrouche na kuongeza:
“Ninajaribu kuwa na matumaini. Tutarekebisha makosa yetu ya mchezo huu na kuongeza umakini katika mechi zijazo, haitakuwa rahisi lakini bado tuna nafasi.”
Kocha wa Morocco, Walid Regragui alisema: “Mechi za kwanza huwa ni ngumu kila mara na tuliiheshimu Tanzania na tumepata ushindi muhimu.
“Tulitaka kufunga mapema na tulipata nafasi, lakini hatimaye bao lilitokana na mpira wa adhabu, baada ya kufunga tulimaliza sehemu ngumu na wakati mwingine katika kipindi cha pili tulikubali kutokuwa na mpira na kusimamia mchezo kama timu kubwa.”
Morocco inaongoza msimamo wa Kundi F kwa pointi tatu ikifuatiwa na DR Congo iliyotoka sare ya bao 1-1 na Zambia inayoshika nafasi ya tatu.
Tanzania inaburuza mkia bila pointi. Januari 21 itapambana na mabingwa wa Afcon 2012, Zambia huku Morocco ikipepetana na DR Congo.
Kimataifa Rais Samia aipongeza Stars
Rais Samia aipongeza Stars
Read also
