Na mwandishi wetu
Kocha mKuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameeleza matumaini aliyonayo kwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Joseph Guede (pichani) akisema atawavusha nchi ya ahadi na kutetea mataji yote ya ndani.
Yanga ilifunga dirisha dogo la usajili kwa kumtambulisha Guede raia wa Ivory Coast kama mrithi wa Hafidh Konkoni ambaye kiwango chake hakikumvutia kocha huyo raia wa Argentina.
Gamondi alisema kupata saini ya mshambuliaji huyo ni sawa na kumaliza tatizo sugu la umaliziaji ambalo limemsumbua tangu aichukue timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.
“Naujua vizuri uwezo wa Guede, ni mshambuliaji aliyekamilika, anajua kufunga lakini hata kutengeneza nafasi kwa wenzake. Binafsi imani yangu ni kubwa kwake, kitu cha msingi kwake ni kuthibitisha hilo kwa kufunga mabao ya kutosha,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema pamoja na uzoefu mkubwa alionao kutokana na kucheza ligi mbalimbali Afrika na Ulaya lakini amemtaka apambane kwenye uwanja wa mazoezi ili kugombea nafasi ya kucheza na washambuliaji waliopo.
Guede mwenye umri wa miaka 29, amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita akitokea timu ya Tuzlaspor FC ya Uturuki.
Yanga kwa ujumla Yanga imesajili wachezaji wengine Shekhan Ibrahim na Agustine Okrah huku ikiachana na Jesus Moloko wakati Crispin Ngushi na Konkoni wakipelekwa kwa mkopo Coastal Union na Cyprus.
