Madrid, Hispania
Real Madrid imeanza kuhamishia nguvu zake katika kuhakikisha inamsajili mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland baada ya kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda Kylian Mbappe asiondoke PSG.
Chanzo kimoja cha habari nchini Hispania kimebainisha hilo ikiwa ni siku moja imepita tangu Rais wa PSG, Nasser Al Khelaïfi aseme kwamba anataka Mbappe abaki katika klabu hiyo ya Ufaransa.
Mkataba wa Mbappe na PSG unafikia ukomo Juni mwaka huu na kwa muda mrefu zimekuwapo habari kwamba mshambuliaji huyo mwenye rekodi ya kuvutia ya mabao ataondoka PSG baada tu ya mkataba wake kumalizika.
Mbappe, 25, mwenyewe amenukuliwa hivi karibuni akisema kwamba hajaamua wapi pa kwenda baada ya PSG ingawa klabu ambazo zinaongoza mbio za kutaka kusaini yake ni Real Madrid na Liverpool.
Kauli ya Al Khelaïfi kumtaka Mbappe abaki PSG pamoja na Mbappe mwenyewe kusema hajaamua lolote huenda ndivyo vilivyoibua hofu Real Madrid kwa imani kwamba mchezaji huyo na rais wa klabu hiyo wameshafanya mazungumzo ya awali.
Kwa kulitambua hilo, Real Madrid wameamua kuelekeza nguvu zao kwa Haaland, 23, ambaye siku za nyuma kulikuwa na habari kwamba katika mkataba wake na Man City kuna kipengele kinachompa nafasi ya kuhamia Real Madrid ingawa kocha wa Man City, Pep Guardiola alipinga jambo hilo.
Hili si jaribio la kwanza kwa Real Madrid kumtaka Haaland na hadi sasa haieleweki ushawishi gani ambao timu hiyo itautumia ili kufanikisha mpango huo.
Kama ilivyo kwa Mbappe, Haaland naye ni mshambuliaji tegemeo wa Man City ambaye msimu uliopita wa 2022-23 mabao yake 52 katika mechi 53 za mashindano yote yaliiwezesha timu hiyo kubeba mataji matatu (treble) ya Ligi Kuu England, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kimataifa Real yamgeukia Haaland, Mbappe hasomeki
Real yamgeukia Haaland, Mbappe hasomeki
Read also
