Na mwandishi wetu
Bondia Hassan Mwakinyo amesema sapoti anayopata kutoka kwa mawaziri wa Serikali ya Zanzibar inampa matumaini ya kufanya vizuri katika pambano lake lililopewa jina la usiku wa Mtata Mtatuzi litakalofanyika Januari 27, mwaka huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mawaziri hao wameahidi kuchangia mamilioni ya viingilio kwa mashabiki watakaoshuhudia pambano hilo ambalo Mwakinyo atapanda ulingoni kupigana na Mbiya Kanku wa DR Congo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa ushirikiano na Peak Time Media, ilielezwa kuwa viongozi hao wameahidi kuchangia pambano hilo kwa ajili ya kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mtandao huo ulieleza kuwa, miongoni mwa viongozi hao ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo aliyechangia meza moja ya watu 10 kwa Sh 1,000,000.
Wengine waliochangia kiasi kama hicho hicho ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaibu Kaduara, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Awadh Maulid, Mkuu wa KMKM, Commodore Msingiri na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid.
Wengine ni Waziri wa Afya, Nassor Mazrui na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hamza Hassan Juma.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Said Marine alisema maandalizi ya pambano hilo yanaendelea vizuri na amewahimiza mashabiki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kujitokeza kwa wingi kufurahia burudani hiyo.
Ngumi Mawaziri Zanzibar wambeba Mwakinyo
Mawaziri Zanzibar wambeba Mwakinyo
Read also
