Na mwandishi wetu
Kiungo wa timu ya taifa, Taifa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema wapo tayari kuiheshimisha Tanzania kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya Afcon inayotarajia kuanza Jumamosi nchini Ivory Coast.
Katika michuano hiyo, Taifa Stars imepangwa Kundi F na timu za Morocco, DR Congo na Zambia na itaanza kampeni ya kusaka taji hilo kwa kucheza na vinara wa soka Afrika, Morocco Januari 17, mwaka huu.
Akizungumza akiwa nchini Ivory Coast, kiungo huyo alisema maandalizi wanayofanya chini ya kocha, Adel Amrouche yamewaongezea ari ya kupambana na kulipa heshima taifa lao licha ya kwamba watu wengi hawawapi nafasi.
“Ukweli kila mchezaji amepania kuipa heshima Tanzania kwa kufanya vizuri kwenye mashindano haya, najua tupo kundi gumu lakini hakuna kinachoshindikana hata hao waliokuwa juu walianza kama sisi kwa hiyo Watanzania waondoe hofu tupo kwa ajili yao,” alisema Fei.
Akijizungumzia yeye binafsi alisema tofauti na ilivyokuwa fainali za mwaka 2019 ambapo alikuwa kijana mdogo kwa sasa yupo fiti na yupo tayari kwa mapambano ya kuipigania nchi yake.
Alisema ana uzoefu wa kutosha kutokana na kucheza mashindano mengi kwenye ngazi ya klabu hivyo matarajio yake mbali na kuiheshimisha Tanzania lakini pia anataka kuitumia michuano hiyo kuonesha kipaji alichonacho.
