Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ amesema anafurahishwa na usajili unaoendelea kufanywa na uongozi wake katika dirisha hili la usajili.
Mashujaa hadi sasa wamekamilisha usajili wa wachezaji wanne ambao ni Mapinduzi Balama, Emmanuel Mtumbuka, Nyenyezi Juma na Abrahman Mussa.
Akizungumza jana, Baresi alisema maboresho yaliyofanyika kwenye kikosi chake yataleta mabadiliko chanya kutokana na aina ya wachezaji walioingia kikosini kwenye dirisha hili la usajili.
“Ukiangalia usajili tuliofanya katika kipindi hiki cha usajili kwa kuongeza wachezaji wazoefu ili watusaidie kutukwamua hapa tulipo ambapo tunapaswa kupambana ili kusogea juu ya msimamo.
“Tuko kwenye nafasi mbaya kwenye msimamo ambayo tunahitaji kufanya jitihada kubwa ili tujikwamue na kutimiza malengo ya kujiondoa chini katika nafasi za msimamo wa ligi,” alisema Baresi.
Alisema hawezi kusema wachezaji waliosajiliwa wanatosha ila anaendelea kuisubiri kamati ya usajili kuona kama watamwongezea wachezaji zaidi.
