Na mwandishi wetu
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema baada ya kukosa nafasi msimu wa 2022/23, msimu ujao nao watakuwa sehemu ya timu 24 zitakazoshiriki michuano ya Africa Football League (AFL).
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC na wanafainali wa Kombe la Shirikisho Afrika walikosa nafasi ya kucheza michuano ya AFL ambapo Ukanda wa Cecafa uliwakilishwa na Simba ambao wako ndani ya timu 10 bora Afrika.
Michuano hiyo ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza Afrika na kuzinduliwa kwenye dimba la Mkapa, Dar es Salaam ilishirikisha timu nane za Al Ahly ya Misri , Esperance ya Tunisia na Wydad ya Morocco zikiwakilisha Kanda ya Kaskazini.
Enyimba ya Nigeria na TP Mazembe ya DRC Congo kutoka Ukanda wa Kati-Magharibi huku Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini, Petro Atletico ya Angola na Simba SC iliwakilisha Afrika Mashariki.
Hersi pia alisema Yanga waliridhia baada ya makubaliano binafsi na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Patrice Motsepe kuwa walichokifanya mwaka jana kuchagua timu shiriki ni kutokana na mazingira ya wakati huo ambapo zilichukuliwa timu nane za kuanzisha AFL.
“Lakini kwa kuwa walikuwa na idadi kamili ya klabu walizokuwa nazo na kwa kauli yake amenidhihirishia kuwa Yanga itashiriki mashindano hayo mwaka huu.
“Kwangu kauli hiyo inatosha na tumeipokea na hatuna sababu ya kufuatilia nini kilichotokea nyuma na tunakubaliana na maamuzi ya viongozi, kilichotokea tuko tayari kushiriki Afrika Football League mwaka 2024,” alisema Hersi.
