Manchester, England
Man United imekubali kumtoa kwa mkopo winga wake Jadon Sancho ambaye sasa atajiunga na klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund ingawa bado kuna mambo ya kuweka sawa ili kukamilisha mpango huo.
Sancho, 23, inadaiwa yuko tayari kurudi Dortmund ikiwa ni takriban miaka miwili na nusu imepita sasa tangu aondoke katika timu hiyo na kujiunga na Man United kwa ada ya Pauni 73 milioni.
Hatua ya mchezaji huyo kuwa tayari kurudi Dortmund imekuja baada ya kujikuta katika wakati mgumu na kocha wake, Erik ten Hag ambaye amemuondoa katika kikosi chake cha kwanza kwa utovu wa nidhamu.
Man United inadaiwa kukubali kumtoa mchezaji huyo kwa mkopo wa miezi sita, makubaliano ambayo yatahusisha sehemu kidogo ya ada pamoja na mchango wao katika mshahara wa Sancho.
Hata hivyo makubaliano hayo bado kusainiwa rasmi na hivyo mchezaji huyo hatoweza kujiunga na kambi ya timu ya Dortmund nchini Hispania katika kipindi hiki cha majira ya baridi.
Sancho amejikuta katika hali hiyo baada ya kukataa kumuomba radhi Ten Hag aliyesema kwamba mchezaji huyo alizembea kwenye mazoezi na hivyo akamuweka kando katika mechi na Arsenal.
Mchezaji huyo hakukubaliana na Ten Hag na kuamua kumjibu kupitia mitandao ya kijamii akisema kwamba kocha huyo aliamua kumtoa kafara na si kweli kwamba alizembea kwa namna yoyote.
Kimataifa United yakubali Sancho aende Dortmund
United yakubali Sancho aende Dortmund
Read also
