Na mwandishi wetu
Yanga leo Alhamisi imeshindwa kutamba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na KVZ, mechi iliyopigwa kwenye dimba la Amaan Complex.
Hayo ni matokeo ya kwanza mabaya kwa Yanga katika michuano hiyo msimu huu baada ya kuweka rekodi ya kuichapa Jamhuri mabao 5-0 na kuilaza Jamus 2-1 katika mechi zake mbili za kwanza.
Ikitumia baadhi ya wachezaji wake wapya na wale wa kikosi cha pili, Yanga ilipata tabu kuipenya ngome ya KVZ na kwa kipindi cha kwanza haikuweza kuonesha kuwa tishio mbele ya timu hiyo.
Yanga ilikianza kipindi cha pili kwa kuongeza nguvu ikiwaingiza, Augustine Okrah, Jesus Moloko na Kibwana Shomari kuchukua nafasi ya Maulid Tamila, Issack Emmanuel na Dennis Nkane.
Mabadiliko hayo bado hayakuweza kuisumbua ngome ya KVZ iliyoongozwa vyema na mlinda mlango, Bashir Darwesh na mabeki, Salum Khamis Gado, Idd Mgeni na Salum Athuman.
Dakika ya 58, Yanga ilipata pigo baada ya Okrah kuumia wakati akiuwahi mpira wa juu na kutolewa nje ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Farid Mussa.
Bado mabadiliko hayo hayakuweza kuipatia Yanga bao ingawa timu hiyo iliongeza uhai ikilisakama lango la KVZ mara kwa mara lakini ukuta imara wa timu hiyo ya Zanzibar uliendelea kuwa kikwazo kwa washambuliaji wa Yanga.
Katika dakika 20 za mwisho KVZ walianza kuja juu wakilisalama lango la Yanga kwa mashambulizi yaliyomuweka katika wakati mgumu kipa wa Yanga, Awesu Kassim na kuibua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo.
Katika dakika za 75, 77 na 80, KVZ walionesha uhai kwa kucheza pasi za uhakika na kufika ndani ya eneo la 18 la Yanga lakini washambuliaji wa timu hiyo walikosa umakini na hivyo kushindwa kubadili matokeo.
Soka KVZ yaigomea Yanga
KVZ yaigomea Yanga
Read also