Na mwandishi wetu
Rais wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Vilabu Afrika, Hersi Said jana Jumatano, alikutana na Rais wa Klabu ya PSG ya Ufaransa, Nasser Al-Khelaifi na kujadili mambo kadhaa kuhusu uhusiano wao wa soka.
Al-Khelaifi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vilabu Ulaya alikutana na Hersi baada ya kumpa mwaliko maalum ikiwamo kuhudhuria mechi ya fainali ya Trophée des Champions iliyochezwa Uwanja wa Parc de Princes, ambapo PSG ilibeba ubingwa ikiichapa Toulouse mabao 2-0.
Pia, baada ya mchezo huo, Hersi alipata fursa ya kukutana na baadhi ya wachezaji nyota wa timu hiyo wakiwemo Marquinhos, Kylian Mbappe na Achraf Hakimi.
Taarifa ya mtandao wa Yanga imeripoti kuwa viongozi hao walipata wakati wa kujadiliana baadhi ya mambo ya soka kama vile jinsi vyama hivyo vikubwa vinavyoweza kujenga uhusiano mzuri wa kusaidia maendeleo ya klabu wanachama wa mabara ya Ulaya na Afrika.

“Hersi alipewa mualiko maalum kutoka Kwa ndugu Nasser Bin Ghanim Al-Khelaifi kwa lengo la kujadili jinsi vyama hivyo vikubwa vinavyoweza kujenga uhusiano mzuri utakaosaidia maendeleo ya vilabu wanachama,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyowekwa leo Alhamisi kwenye vyanzo vya habari vya klabu ya Yanga.