Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amesema ugeni wake Tanzania imekuwa chanzo cha timu hiyo kupata matokeo kwa tabu kwenye mechi za Ligi Kuu NBC.
Benchikha alisema hiyo ni kutokana na kutojua vizuri mifumo ambayo inatumiwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu NBC, hivyo kujikuta wanatumia nguvu nyingi kupata ushindi.
“Kama ningekuwa hapa (Tanzania) miezi mitatu au sita iliyopita, hili lisingekuwepo sababu ningejua mifumo inayotumiwa na timu zote lakini kwa sasa ni ngumu ndio maana mara nyingi tunakitumia kipindi cha kwanza kuwasoma wapinzani,” alisema Benchikha.
Alisema pamoja na hivyo lakini anafurahi kuona vijana wake wanashika kwa haraka anachowaelekeza mazoezini na ndio maana wanapata ushindi.
Alisema anachokifanya kwa sasa ni kufundisha vitu viwili kwa wakati mmoja, kwanza kusoma mbinu za wapinzani na pili kuwapa wachezaji wake mbinu mbadala zitakazowapa ushindi.
Benchikha pia alisema kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Tanzania, ameshuhudia timu nyingi zikionesha uwezo mkubwa na hiyo inatokana na taifa hili kuwa na vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka.
Benchikha aliyetua Simba akitokea USM Alger ndio kocha ghali zaidi Tanzania anayeshikilia rekodi ya kubeba makombe mawili ya Caf, ambayo ni Kombe la Shirikisho Afrika na Super Cup msimu uliopita.
Soka Benchikha ataja ugumu anaoupata Simba
Benchikha ataja ugumu anaoupata Simba
Read also
