Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Ihefu, Mecky Maxime amewataka mabosi wa timu hiyo watarajie mambo makubwa kutokana na mifumo ya kisasa anayoipandikiza kwa wachezaji wake.
Akizungumza leo Jumatano, kocha huyo alisema timu hiyo ina wachezaji wazuri isipokuwa kilichokuwa kinawasumbua kutopata matokeo mazuri ni mfululizo wa vipigo.
“Kufungwa mfululizo kumevuruga saikolojia ya wachezaji, baada ya kukabidhiwa timu kitu cha kwanza nilichoanza nacho ni kujenga saikolojia zao na kupandisha ari ya upambanaji ili waweze kufanya vizuri,” alisema Maxime.
Kocha huyo alisema mipango yake ni kuiondoa Ihefu nafasi ya 13 hivi sasa kwenye Ligi Kuu NBC na kuipandisha nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Alisema anatambua ugumu uliopo kwenye ligi ya msimu huu lakini anajivunia uwezo wa wachezaji wake pamoja na wasaidizi wake hakuna kitu kitashindikana.
Ihefu ambayo hadi sasa imeshatimua makocha wawili ambao ni Zuberi Katwila na Moses Basena, ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 13 katika michezo 14.
