Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Azam FC, Youssoufa Dabo ameeleza kufurahishwa na ubora uliooneshwa na wachezaji wake katika michezo mitatu ya hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi na sasa akili zao wanazihamishia katika robo fainali.
Azam ilianza michuano ya Mapinduzi kwa kulazimishwa suluhu na Mlandege kabla ya kuzinduka na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chipukizi United na kuhitimisha hatua ya makundi kwa kuichapa Vital’O mabao 3-1.
Mara ya mwisho Azam kushinda ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ilikuwa mwaka 2019 waliposhinda kwa kuichapa Simba mabao 2-1.
Dabo alisema ukurasa wa makundi umefungwa, sasa wanaangalia hatua inayofuata ambayo inahitaji umakini kwani unapofanya makosa unaadhibiwa na kuyaaga mashindano.
“Wachezaji wamefanya kazi nzuri katika michezo mitatu mfululizo na kufanikiwa kumaliza hatua ya makundi tukiwa vinara hivyo tuna kazi ya kufanya ili kusonga mbele.
“Malengo yetu ni kutwaa ubingwa wa mashindano haya ambayo yanajumuisha timu nzuri lakini kikosi bora ndicho kitaenda kutwaa kombe, naamini vijana wangu hawataniangusha,” alisema Dabo raia wa Senegal.
