Na mwandishi wetu
Bao la Nickson Kibabage lililopatikana katika dakika za nyongeza limeipa Yanga ushindi wa mabao 2-1 na kuiokoa kutoka sare ya bao 1-1 na Jamus ya Sudan Kusini katika mechi ya Kombe la Mapinduzi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Jumanne usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Kibabage alifunga bao hilo katika dakika saba za nyongeza (dk 96) baada ya kupenyezewa pasi na Clement Mzize.
Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 16 ya mchezo huo mfungaji akiwa ni Farid Mussa kwa shuti la mpira wa adhabu ambalo lilikwenda moja kwa moja wavuni.
Jamus, walisawazisha bao hilo dakika ya 41 mfungaji akiwa ni David Vincente ambaye aliinasa pasi ya Yusuf Mursali aliyempiga chenga kipa Abuutwalib Mshery wa Yanga kabla ya kutoa pasi iliyozaa bao.
Mshery alilazimika kutoka langoni mwake kwa lengo la kwenda kumdhibiti Mursali baada ya safu ya ulinzi ya Yanga kuyumba.
Katika kipindi cha pili, Jamus walionekana kucheza kwa malengo, wakifanya mashambulizi machache lakini makini katika kuzuia mashambulizi ya Yanga hasa baada ya timu hiyo kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili.
Jamus walifanikiwa katika mpango huo kabla Kibabage hajabadili matokeo sekunde kadhaa kabla ya mpira kumalizika na kuifanya Yanga itoke uwanjani na pointi tatu na mabao mawili na kufikisha jumla ya pointi sita na mabao saba katika mechi zake mbili za Kombe la Mapinduzi.
Katika mechi nyingine iliyochezwa mapema leo, Azam FC walitokana uwanjani na ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Vitalo ya Burundi.
Soka Kibabage aokoa jahazi Yanga
Kibabage aokoa jahazi Yanga
Read also
