Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti hatimaye amedhihirisha kwamba hana mpango wa kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Brazil baada ya kuongeza mkataba na Real Madrid.
Ancelotti alihusishwa na mipango ya kusaini mkataba kuinoa timu ya Brazil lakini habari zilizopatikana leo Jumamosi ni kwamba kocha huyo ameongeza mkataba na Real Madrid hadi mwaka 2026.
“Real Madrid na Carlo Ancelotti wamefikia makubaliano ya kuongeza mkataba hadi Juni 30, 2026,” ilieleza taarifa ya Real Madrid.
Julai mwaka huu ilielezwa kwamba kocha huyo mwenye umri wa miaka 64 alikuwa anaandaliwa kuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu ya Brazil lakini hatua yake ya kuongeza mkataba inalifanya suala hilo kuwa gumu au ambalo halina nafasi.
Katika kumuandalia Ancelotti nafasi hiyo, Shirikisho la Soka Brazil (CBF) lilimtangaza Fernando Diniz kuwa kocha wa muda huku matumaini yakiwa ni kumsubiri Ancelotti achukue jukumu hilo kwenye fainali za Copa America 2024.
Inadaiwa kwamba Ednaldo Rodriguez ambaye alikuwa rais wa CBF wakati huo alifanya mazungumzo kadhaa na Ancelotti ambaye naye aliwahi kunukuliwa akisema kazi ya kuinoa Real Madrid itakuwa ya mwisho kwake kwenye kazi ya ukocha wa soka.
Hoja ya Rodriguez kumtaka Ancelotti ainoe timu ya taifa ya Brazil hata hivyo ilikumbana na upinzani kwa kilichodaiwa kwamba kumchukua kocha kutoka nje ya Brazil ni kuwadharau makocha wazawa.
Hoja nyingine zilidai kwamba Ancelotti haujui utamaduni wa soka la Brazil na hivyo isingekuwa sahihi kumpa kibarua cha kuinoa timu hiyo.
Mipango ya kumpa kibarua Ancelotti imechangiwa na matokeo yasiyopendeza ya timu ya taifa ya Brazil hasa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 na ikaonekana umuhimu wa kutafuta kocha kutoka nje ya taifa hilo na ndipo jina la Ancelotti lilipochomoza.
Kimataifa Ancelotti afuta mpango wa kuinoa Brazil
Ancelotti afuta mpango wa kuinoa Brazil
Read also
