Na mwandishi wetu
Azam FC wapo katika mchakato wa kumsajili kipa namba moja wa Tabora United, John Noble ili kuziba nafasi ya makipa wake wawili Abdulah Idrissu na Ally Ahmada ambao kwa sasa ni majeruhi.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Yossouf Dabo alisema sababu ya kumchagua kipa huyo raia wa Nigeria ni kutokana na uwezo aliouonesha katika mechi kadhaa alizoichezea timu yake kwenye Ligi Kuu NBC.
“Noble ni kipa mzuri, hilo halina ubishi na hakuna timu haipendi kuwa na kipa wa aina yake ndio maana naushawishi uongozi tuweze kumpata ili atusaidie kufikia malengo yetu na ukizingatia hatutokuwa na makipa wetu tegemezi kutokana na majeraha waliyokuwa nayo,” alisema Dabo.
Kocha huyo alisema mbali nafasi ya kipa pia watafanya maboresho kwa kusajili wachezaji wasiozidi watatu kwenye dirisha hili dogo la usajili akiwemo mshambuliaji na beki wa kulia.
Alisema baadhi ya wachezaji hao tayari wameanza mazungumzo nao ili kukamilisha usajili wao na anaamini kabla ya kumalizika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar watakuwa wamekamilisha usajili wa wachezaji hao.
Dabo alisema anataka kuwa na kikosi chenye wachezaji wanaolingana uwezo ili kupata uhakika wa kile walichokikusudia ifikapo mwisho wa msimu huu ambacho ni ubingwa wa Ligi Kuu NBC.
Azam kwa sasa ndio vinara katika ligi hiyo wakikusanya pointi 31 katika michezo 13 waliyocheza na wamesaliwa na mechi mbili kumaliza mzunguko wa kwanza.
Soka Azam yamtaka kipa Noble wa Tabora
Azam yamtaka kipa Noble wa Tabora
Read also
