Manchester, England
Bilionea wa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe (pichani) amekubali kununua asilimia 25 ya hisa za klabu ya Manchester United kwa Pauni 1.03 bilioni kupitia kampuni yake ya Ineos ambayo sasa itasimamia maendeleo ya soka la klabu hiyo.
Katika mpango huo uliotangazwa rasmi jana Jumapili, bilionea huyo mwenye umri wa miaka 71 pia anatarajia kutumia Pauni 236 milioni kwa uwekezaji katika uwanja wa klabu hiyo wa Old Trafford.
Tangazo la bilionea huyo, limekuja ikiwa ni miezi takriban 13 imepita tangu wamiliki wa klabu hiyo Familia ya Glazer kutangaza kusudio lao la kumtafuta mtu wa kumuuzia hisa katika klabu hiyo ambayo waliinunua mwaka 2005 kwa Pauni 790 milioni.
Tangu Familia ya Glazer kutoa tangazo hilo, mtu mwingine aliyeonekana kuwa mstari wa mbele kutaka kuinunua klabu hiyo ni bilionea wa Qatar, Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani ambaye hata hivyo Oktoba mwaka huu alitangaza kufuta mpango wa kuinunua klabu hiyo kwa asilimia 100.
Man United imekuwa katika kipindi kigumu, haijashinda taji la Ligi Kuu England tangu mwaka 2013 huku mashabiki mara kwa mara wamekuwa wakiandamana kupinga umiliki wa Familia ya Glazer.
Wakati tararibu za mwisho za mauziano hayo zikiendelea, taarifa ya Kampuni ya Ineos iliyopatikana ilieleza kuwa inafahamu kazi ngumu na changamoto zilizo mbele yao na imejipanga kukabiliana nazo ili kuweka mambo sawa.
“Shauku yetu ya pamoja ipo wazi, sote tunataka kuona Manchester United ikirudi kule inapopaswa kuwa, kwenye kilele cha soka la England, Ulaya na duniani,” ilieleza taarifa ya Ineos.
Sir Jim ambaye ni mzaliwa wa jiji la Manchester pia ni shabiki wa klabu hiyo, mwaka jana alidhamiria kununua hisa katika klabu ya Chelsea lakini mpango huo ulikwama ndipo alipoamua kuelekeza nguvu zake Man United.
Kampuni yake ya Ineos si ngeni katika masuala ya michezo hivyo mashabiki wamekuwa na matarajio makubwa na bilionea huyo kuweka mambo sawa katika klabu hiyo ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa ikiyumba.
