Yaounde, Cameroon
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon, Roger Milla ameigeukia biashara ya utunzaji na usafi wa mazingira kwa kukusanya taka za plastiki, kuzirudisha kiwandani na kuzalisha vitofali na bidhaa nyingine.
Lengo la mradi huo wa Roger Milla ni kupunguza takataka za plastiki mitaani ambazo pia zinachangia uharibifu wa mazingira na kusababisha mafuriko pamoja na kutoa ajira kwa vijana.
Cameroon ni nchi mojawapo inayoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mafuriko sababu mojawapo ikiwa ni mvua lakini pia kuwapo kwa taka za plastiki zinazoziba mifereji hivyo mradi huo unatajwa kusaidia kupunguza tatizo la mafuriko.
Mradi huo upo katika jiji la Yaounde tangu mwaka 2017 na umeajiri vijana zaidi ya 700 ambazo si ajira rasmi lakini wapo wengine zaidi ya 20 wenye ajira za kudumu na hadi sasa tayari wamekusanya tani zaidi ya 50 za takataka za plastiki.
Baada ya jiji la Yaounde, Roger Milla yuko katika hatua za mwisho za kufungua mradi kama huo katika jiji la Douala na baada ya hapo mpango wake ni kufungua mradi huo nje ya Cameroon katika nchi za Benin na Burkina Faso huku lengo likiwa ni kuajiri vijana zaidi ya 2,500.
Roger Milla anakumbukwa kwa kuiwakilisha Cameroon kwenye fainali za soka za Kombe la Dunia mwaka 1990 na kuifungia mabao manne yaliyoiwezesha timu hiyo kuweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufikia hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Wakati Roger Milla akiweka rekodi hiyo alikuwa na miaka 38 na miaka minne baadaye wakati huo akiwa na miaka 42 pia aliitwa kwenye timu ya taifa ya Cameroon iliyofuzu na kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Marekani.
Roger Milla mbali na kuweka rekodi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mara mbili akiwa na umri mkubwa, anakumbukwa kwa namna alivyokuwa akishangilia bao alilofunga kwa kwenda kwenye kibendera na kukata mauno.
GreenSports Roger Milla ageukia ujasiriamali, utunzaji mazingira
Roger Milla ageukia ujasiriamali, utunzaji mazingira
Related posts
Read also
