Na Hassan Kingu
Uamuzi wa Simba kumsimamisha kiungo wake, Clatous Chota Chama umeacha maswali miongoni mwa mashabiki kuhusu hatma ya mchezaji huyo huku wengine wakikimbilia kumhusisha na Yanga.
Uongozi wa Simba jana Alhamisi ulitoa taarifa ya kusimamishwa kwa wachezaji wawili Chama pamoja na Nassor Kapama kwa kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu wa wachezaji hao.
Taarifa hiyo hata hivyo haikufafanua ni vitendo gani vya utovu wa nidhamu vilivyofanywa na wachezaji hao, badala yake ilisisitiza juu ya watumishi wa klabu ya Simba kuzingatia misingi ya maadili na nidhamu.
Baadhi ya mijadala inayoendelea kisikika hasa mitandaoni imekuwa ni kuhusu Chama pekee, hatma yake, nini hasa alichokifanya, kwa nini hakuvumiliwa na mengineyo.
Moja ya hoja ambayo imeendelea kujadiliwa ni kwamba uamuzi wa kumsimamisha Chama ni wa muda tu, ni kama vile klabu inatingisha kiberiti lakini mchezaji huyo atajadiliwa na kamati ya nidhamu kama ilivyoelezwa na suluhisho litafikiwa na mwishowe ataendelea kuitumikia Simba.
Pia ipo hoja kwamba mchezaji huyo amekuwa na tatizo la utovu wa nidhamu kwa muda mrefu na amekuwa akivumiliwa na makocha wake lakini kocha wa sasa, Abdelhak Benchikha ameshindwa kumvumilia.
Katika hali ya kawaida ni vigumu kwa Simba kuruhusu au kukubali kuachana na mchezaji wa hadhi ya Chama ambaye tayari amedhihirisha umuhimu wake kwenye Ligi Kuu NBC pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inapigania kulibeba taji la Ligi Kuu NBC lakini pia inapambana na ipo katika hatua nzuri kwenye mbio za kuwania kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kote huko nafasi na mchango wa Chama unahitajika.
Ujasiri wa kuachana na mchezaji huyo katika mazingira yoyote yale bado hauwezi kuwa na nafasi na kama italazimika kufanya hivyo basi tatizo la utovu wa nidhamu analodaiwa kulifanya Chama linaweza kuwa kubwa na ambalo halivumiliki.
Matatizo ya utovu wa nidhamu wanayohusishwa nayo wachezaji mara nyingi yanakuwa ya kufanana kama vile nidhamu ya kutojali muda, kutofika mazoezini kwa wakati au kutofika kabisa na mara nyingi hutokea mara moja moja hivyo kamwe hayawezi kuwa sababu ya klabu kuachana na mchezaji tena mchezaji mwenyewe Chama.
Hadithi inayosikika mitandaoni ya kuharakia kumhusisha Chama na Yanga huenda imetengenezwa na Yanga kwa nia ya kuwavuruga Simba lakini bado si jambo rahisi kwa Simba kukubali kuachana na Chama au kuwa tayari kumuona Chama akielekea Yanga.
Soka Chama aibua maswali baada ya kusimamishwa
Chama aibua maswali baada ya kusimamishwa
Read also