Na mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ amesema anaamini kiwango ilichonacho Simba kwa sasa, itaifunga Asec Mimosas kwenye mchezo unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
MwanaFA ameyasema hayo baada ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad AC, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kupata ushindi wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya mechi nne.
Alisema sehemu iliyokuwa ngumu kupata ushindi kwa Simba ugenini ilikuwa ni Morocco dhidi ya Wydad ambapo Simba ilifungwa bao 1-0 lakini anaamini nchini Ivory Coast itakuwa rahisi dhidi ya Asec.
“Kiwango kikibaki hivihivi naamini Simba itapata alama tatu, mahali pagumu kupata alama tatu palikuwa Wydad, Morocco kule na ilikuwa chupuchupu ipatikane angalau moja ila tu mpira una matokeo yake na chochote kinatokea.
“Lakini sina wasiwasi kabisa na kiwango cha Simba dhidi ya Asec, naamini pointi tatu zitachukuliwa tu kulekule ugenini,” alisema Mwinjuma ambaye pia ni shabiki mkubwa wa Wekundu hao.
Simba inatarajia kukutana na upinzani mkubwa katika mchezo huo utakaopigwa Februari 23, mwaka huu kutokana na rekodi ya Asec ya kutopoteza mechi yoyote ya nyumbani katika michuano hiyo msimu huu mpaka sasa.
Katika Kundi B, Asec inaongoza kwa pointi 10, Simba ya pili ikiwa na pointi tano wakati Jwaneng Galaxy ya Botswana ni ya tatu kwa pointi nne na Wydad inaburuza mkia ikiwa na pointi tatu.
