Na mwandishi wetu
Licha ya winga wa Yanga, Skudu Makudubela (pichani) kukiri kuwa Ligi ya Tanzania ni ngumu lakini ameahidi kuendeleza moto wa kufunga mabao msimu huu.
Skudu amezungumza hayo baada ya juzi kufanikiwa kuifungia Yanga bao la kwanza tangu atue Jangwani mwanzoni mwa msimu huu, walipoumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.
“Ligi ya Tanzania ni nzuri na ina ushindani mkubwa sana, nafikiri kila timu inayocheza na Yanga inapambana kwa kadri iwezavyo kuonesha kuwa mshindani hivyo kila.mechi kwetu tunahitaji kucheza kwa bora wa hali ya juu.
“Nashukuru Mungu kufunga bao la kwanza, haikuwa kitu rahisi kwa kweli maana pia ilikuwa mechi yangu ya kwanza nacheza kwa dakika 90 lakini nimefurahi kufunga na natazamia kufunga zaidi katika siku za usoni msimu huu,” alisema Skudu.
Winga huyo raia wa Afrika Kusini aliyewahi kuzitumikia Orlando Pirates, Mamelodi Sundowns, Chippa United na nyinginezo, ametua Yanga akitokea Marumo Gallants.
Skudu bado anapambana kutafuta namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kutokana na ushindani uliopo kwenye kikosi hicho licha ya ufundi alionao.