Na mwandishi wetu
Taarifa mpya ni kuwa uongozi wa timu ya Mashujaa na kocha wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ wamekaa mezani kuyamaliza na sasa kocha huyo ataendelea kukinoa kikosi hicho.
Pande hizo mbili zimelazimika kukutana hivi karibuni baada ya wiki iliyopita, Baresi kuandika barua ya kuachia ngazi kutokana na matokeo mabovu mfululizo ya timu hiyo iliyopanda kushiriki Ligi Kuu NBC msimu huu.
Akizungumza na GreenSports, Baresi alieleza kuwa kwa sasa hakuna tena mipango ya kuihama Mashujaa yenye maskani yake Kigoma baada ya kukutana na kuzungumza na uongozi.
“Kama ulivyosikia, niliwapa barua viongozi ya kujiuzulu lakini baadae nilikutana na uongozi, tukazungumza na kukubaliana baadhi ya vitu na ieleweke tu kwamba tumeyamaliza na tunaendelea kuipigania Mashujaa,” alisema Baresi.
Alisema kwa sasa wako kwenye maandalizi kabambe ya kuhakikisha wanapata matokeo kwenye mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Mashujaa itaingia uwanjani ikitafuta ushindi iliyoukosa katika mechi nane mfululizo zilizopita, wakipoteza mechi sita na kuambulia sare mbili na sasa wanashika nafasi ya 15 kwa pointi tisa huku Mtibwa ikiburuza mkia katika nafasi ya 16 ikiwa na pointi tano pekee.
