Milan, Italia
Mshambuliaji wa zamani wa AC Milan, Zlatan Ibrahimovic ambaye amestaafu soka, amerudi kwa mara nyingine katika klabu hiyo baada ya kuteuliwa kuwa mshauri mkuu wa wamiliki na viongozi wa klabu.
Ibrahimovic, 42, sasa anakuwa amerudi katika klabu hiyo kwa mara ya tatu ikiwa imepita takriban miezi sita tangu atangaze kustaafu soka.
Katika miaka 24 ya kwenye soka, Ibrahimovic mbali na AC Milan pia amezichezea kwa mafanikio klabu mbalimbali barani Ulaya za Juventus, Barcelona, Inter Milan, PSG pamoja na Man United akiwa na rekodi ya kubeba mataji ya ligi katika nchi nne tofauti.
Kampuni ya RedBird ambao ndio wamiliki wa AC Milan tangu Agosti mwaka jana walipoinunua kwa Pauni 1 bilioni, wamemteua Ibrahimovic ambaye pia atakuwa mshirika wao katika michezo yote, vyombo vya habari na masuala ya burudani ndani ya yote hiyo imo pia klabu ya AC Milan.
Ibrahimovic kinara wa mabao kwenye timu ya taifa ya Sweden, alijiunga na AC Milan kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alisema mapenzi yake na Rossoneri (AC Milan) hayawezi kuisha.
“Mapenzi yangu kwa Rossoneri hayawezi kuisha na fursa hii ya kuwa sehemu katika mambo ya baadaye katika namna iliyo bora ni kitu ambacho niliishia kukiota,” alisema Ibrahimovic.
Alisema uamuzi wa kumteua katika wadhifa huo si wa kuuchukulia kirahisi, ni jambo muhimu kwake na familia yake kwani alikuwa akifikiria kwa muda mrefu maisha baada ya kustaafu soka na amejikuta mwenye furaha kwa kuwa pamoja kama mwanachama katika safari ya RedBird na AC Milan.
