Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga ikiwa ugenini nchini Ghana, leo Ijumaa imetoka sare ya bao 1-1 na Medeama katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja wa Babayara.
Matokeo hayo ya ugenini yanaifanya Yanga kuendelea kuburuza mkia katika kundi lake ikiwa na pointi mbili katika mechi tatu ikiwa imepoteza mechi moja na kutoa sare mbili.
Al-Ahly ya Misri ambayo nayo leo imetoka sare ya bila kufungana na CR Belouizdad ndiyo inayoshika usukani wa kundi hilo ikiwa na pointi tano ikifuatiwa na Belouizdad na Madeama inashika nafasi ya tatu, timu zote hizo kila moja ina pointi nne na zinapishana kwenye uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mechi ya leo mambo yaliwaharibikia Yanga dakika ya 27 Medeama walipopata bao la penalti iliyotolewa baada ya Dickson Job kumchezea rafu winga Derick wa Madeama na Jonathan Sowah akaujaza mpira wavuni.
Zikiwa zimebakia dakika 10 timu kwenda mapumziko, Pacome Zuouzoua aliisawazishia Yanga bao baada ya kuonesha juhudi binafsi kwa kuukokota mpira na kuwafuata mabeki wa Medeama ambao walijichanganya kwa kurudi nyuma.
Zouzoua ambaye pia ndiye aliyefunga bao la kusawazisha katika mechi ya Yanga na Al Ahly, akautumia mwanya huo kulisogelea zaidi lango la Medeama na kufumua shuti la mguu wa kushoto lililomshinda kipa Felix Kyei.
Kocha wa Yanga Manuel Gamondi alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Clement Mzize na nafasi yake kuchukuliwa na Aziz Ki na Kennedy Musonda ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Hafiz Konkoni, mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Katika mechi hiyo wachezaji wa Yanga, Ibra Bacca na Job walipewa kadi za njano kwa kucheza rafu pamoja na kocha wao Gamondi ambaye alipewa kadi hiyo kwa kilichoonekana kama kuzozana na waamuzi wasaidizi.
..
