Na mwandishi wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amelielekeza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha ifikapo Januari, mwakani kila klabu ya Ligi Kuu NBC iwe imewakatia bima ya afya wachezaji wake.
Akizungumza Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Soko la Bima kwa Mwaka 2022, Dk Ndumbaro alisema kwa kazi ya wachezaji jinsi ilivyo wanahitaji bima wakiwa ndani na nje ya uwanja.
“Nakupa maelekezo Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha kuwa timu zote ni lazima ziwe na bima na suala hili liingie kwenye kanuni ili kuwalinda wachezaji wafanye vizuri zaidi na kuleta mafanikio katika nchi,” alisema.
Dk Ndumbaro alisema bima katika michezo ni kubwa sana kuliko vile Watanzania wanavyodhani na kwamba sekta ya michezo ina fedha nyingi sana, watu wengi na wadau wengi na kuhimiza kampuni za bima kuangalia upande huo na kuwatumia kama sehemu ya kujitangaza.
Akitolea mfano wa timu zinazowakilisha vyema ikiwemo za taifa ambazo zinafanya vizuri na klabu za Simba na Yanga ambazo zimefuzu kwa mara ya kwanza kwa pamoja hatua ya makundi zinaweza kutumika vyema na zikawatangaza kimataifa.