Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ametinga kwenye hatua ya mwisho ya tatu bora ya kuwania tuzo ya kocha bora wa Afrika inayotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Makocha wengine wawili wanaochuana na Benchikha ni kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui na kocha wa timu ya taifa ya Senegal, Aliou Cisse.
Benchikha raia wa Algeria amefanikiwa kupenya kwenye tatu bora kutokana na mafanikio yake msimu uliopita alipokuwa na klabu ya USM Alger ambayo aliipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Yanga SC na kutwaa ndoo ya Caf Super Cup dhidi ya Al Ahly.
Taarifa hiyo iliyowekwa na mtandao rasmi wa Caf leo Alhamisi pia imewataja walioingia tatu bora kwenye tuzo ya mchezaji bora Afrika ni Mohamed Salah wa Liverpool raia wa Misri, Achraf Hakimi raia wa Morocco anayekipiga PSG na Victor Osimhen kutoka Nigeria anayekipiga Napoli.
Tuzo ya mchezaji bora wa ndani Afrika inawaniwa na Peter Shalulile wa Mamelodi Sundowns, Percy Tau wa Al Ahly na Fiston Mayele wa Pyramids ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho kwa kufunga mabao saba akiwa na timu ya Yanga.
Na tuzo ya mchezaji bora wa kike Afrika inawaniwa na Asisat Oshoala wa Nigeria anayeichezea Barcelona, Thembi Kgatlana wa Afrika Kusini anayekipiga Louisville FC na Mnigeria, Barbra Banda ambaye ni nahodha wa Shanghai Shengli.
Tuzo nyingine ni ya kipa bora wa mwaka inayogombaniwa na kipa wa Man United, Andre Onana wa Cameroon, Mohamed El Shanawy anayeidakia Al Ahly ya kwao Misri na Yassine Bounou wa Morocco anayeidakia Al Hilal ya Saudi Arabia.
Nayo Yanga iliyotinga kwenye tano bora ya tuzo ya klabu bora ya mwaka, imeng’oka kwenye tatu bora na kuziacha klabu za Al Ahly, Mamelodi Sundowns na Wydad AC zikiwania kipengele hicho.
Katika tuzo ya timu bora ya taifa kwa wanaume zinazowania ni Morocco, Senegal na Gambia huku tuzo ya timu bora ya taifa kwa wanawake ikigombaniwa na Morocco, Nigeria na Afrika Kusini.
Halfa ya utolewaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Desemba 11 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Palais des Congres, Movenpick mjini Marakesh, Morocco.
Kimataifa Benchikha yumo tuzo ya kocha bora Afrika
Benchikha yumo tuzo ya kocha bora Afrika
Read also
