Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amewataka wenye mamlaka katika klabu hiyo kumuamini katika harakati za kuirudisha timu hiyo katika mafanikio yake ya zamani.
Ten Hag ametoa kauli hiyo akiwa anaandamwa na matokeo mabaya kikiwamo kipigo cha mwisho cha bao 1-0 dhidi ya Newcastle Jumapili iliyopita kikiwa ni kipigo cha 10 katika mechi 21 za msimu huu.
Hapo hapo habari za ndani zinadai kwamba baadhi ya wachezaji hawafurahishwi na mfumo wa kocha huyo kuanzia mazoezini hadi mbinu anazotumia kwenye kikosi chake.
Katikati ya matukio yote hayo Man United imeingia katika mgogoro na baadhi ya vyombo vya habari hadi kuwazuia baadhi ya waandishi kwenye mikutano yake kwa madai ya kutoipa nafasi klabu hiyo kutoa ufafanuzi wa habari hasa zile mbaya zinazorushwa na vyombo hivyo.
Man United leo Jumatano usiku itaumana na Chelsea katika mechi nyingine ya EPL, mechi ambayo inachezwa wakati Ten Hag akiwa kwenye kipindi kigumu, timu yake inashika nafasi ya saba EPL, imetolewa kwenye mbio za taji la EFL na inashika mkia katika kundi lake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ten Hag hata hivyo ameendelea kujiamini akiwataka mabosi wake wamuamini kwamba ana uwezo wa kuirudisha timu kwenye mstari wa mafanikio kama watakuwa wamoja na kushikamana na mipango na malengo yao.
“Najua tutafika huko tunakotaka kufika, kwa sababu, angalieni rekodi zangu kila mahali nilipokuwa katika misimu yote, ninafanikisha malengo yangu,” alisema Ten Hag.
Kocha huyo pia alipinga hoja inayozungumzwa kwamba kuna wachezaji wasiokubaliana na mbinu zake ingawa alisema kwamba wapo wawili ambao walimtamkia hilo lakini walio wengi wanajitoa kwa ajili ya timu na kushikamana na mfumo anaoufanyia kazi na ndicho wanachokitaka.
