Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa KMC, Abdulhamid Moalin amesema mechi yao ya kesho Alhamisi dhidi ya Azam FC itakuwa ni kipimo tosha kwa kikosi chake kugombea nafasi nne za juu msimu huu.
Moalin aliyewahi kuinoa Azam mwanzoni mwa msimu uliopira alisema hiyo ni kutokana na ubora wa kikosi cha timu hiyo pamoja na uwekezaji mkubwa walioufanya msimu huu.
“Najua mazingira yote ya Azam ndio maana nasema mchezo wetu wa kesho dhidi yao utakuwa mgumu lakini tumejiimarisha kuwaonesha kwamba na sisi si timu ndogo, kitu cha msingi tunachohitaji kutoka kwao ni pointi tatu,” alisema Moalin.
Kocha huyo alisema anajivunia uimara wa safu yake ya ushambuliaji na kiungo ambayo imekuwa ikiimarika katika kila mchezo lakini pia safu yake ya ulinzi imekuwa ikifanya kazi nzuri ndio maana wameruhusu mabao machache katika mechi za karibuni.
Alisema kwake utakuwa mchezo muhimu kushinda sababu timu anayokutana nayo anajua namna ya kuwadhibiti na kupata matokeo licha ya kwamba watakuwa kwenye uwanja waliouzoea wa Azam Complex, Dar es Salaam.
KMC ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 19 sawa na timu za Simba iliyopo nafasi ya tatu na Singida Fountain Gate waliopo nafasi ya nne ambao wamekaa juu kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Soka Moalin: Azam kipimo tosha kwetu
Moalin: Azam kipimo tosha kwetu
Read also
