Na mwandishi wetu
Timu ya Simba imeondoka leo Jumanne kuelekea Marakesh, Morocco kwa ajili ya mchezo wao wa tatu wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC, Jumamosi hii.
Simba imeondoka majira ya saa 9 alasiri na kikosi cha wachezaji 23 tayari kwa ajili ya kuipambania timu hiyo kutafuta ushindi wake wa kwanza katika hatua hiyo ya makundi.
Tayari Simba imechacheza mechi mbili za Kundi B na kuambulia sare dhidi ya ASEC Mimosas, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na ule wa ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema: “Safari yetu itakuwa Qatar kisha Casablanca halafu Marakech ambapo tunatarajia kufika kesho Jumatano, hivyo tutafanya mazoezi kwa siku mbili kabla ya mchezo wenyewe Jumamosi.
“Maandalizi yanakwenda vizuri kwamba mratibu wetu, Abbas Ally tayari yupo Morocco kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa tukifika kule na upande wa ufundi kocha Abdelhak Benchikha ameendelea kuwaweka sawa vijana kuhakikisha tunapata matokeo dhidi ya Wydad” alisema Ally.
Wekundu hao wanatarajia kuumana na Wydad kwenye Uwanja wa Marrakesh, mjini Marrakesh kuanzia saa 4.00 usiku.
Wenyeji Wydad wanaburuza mkia katika kundi hilo bila ya pointi baada ya kufungwa na Jwaneng na ASEC, hivyo mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu kwa kuwa nao wanatafuta ushindi wa kwanza kama ilivyo Simba.
Nao wawakilishi wengine wa michuano hiyo, Yanga walioanza safari hiyo leo alfajiri wamefika salama mjini Accra, Ghana kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Medeama Ijumaa hii utakaopigwa kwenye Uwanja wa Baba Yara, Kumasi kuanzia saa 1.00 jioni.
Akizungumza na GreenSports kutoka Accra, meneja wa habari na mawasiliano Yanga, Ally Kamwe alisema wamefika salama katika mji huo na wanatarajia kuunganisha safari yao mpaka Kumasi kwa ajili ya mechi hiyo huku wakiomba dua za mashabiki wa timu hiyo kwa ajili ya matokeo mazuri nchini humo.
“Kila kitu kimeenda sawa, tumefika hapa (Accra) majira ya saa tano asubuhi na tunatarajia kutoka hapa kuelekea Kumasi ambapo kwa safari ya ndege ni dakika 45 mpaka huko ambako ndiko kutachezwa mechi yenyewe,” alisema Ally.
Yanga inayoburuza mkia kwa pointi moja kwenye Kundi D inatafuta pia ushindi wa kwanza baada ya kufungwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ugenini kabla ya kutoa sare ya bao 1-1 na Al Ahly, Uwanja wa Mkapa.
Al Ahly inaongoza kundi hilo kwa pointi nne ikifuatiwa na Belouizad yenye pointi tatu sawa na Medeama ambayo iko nafasi ya tatu kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
