London, England
Klabu ya Manchester City imekutwa na hatia na Chama cha Soka England (FA) kwa kosa la kushindwa kuwazuia wachezaji wake kumzonga mwamuzi wa mechi yao na Tottenham iliyoisha kwa sare ya 3-3.
Wachezaji hao walimzonga mwamuzi, Simon Hooper baada ya kuwapa mpira wa adhabu katika dakika tano za nyongeza wakati tayari waliuwahi mpira na walitarajia angeruhusu mchezo uendelee na ilionekana kama Jack Grealish alikuwa akielekea kuipatia bao timu hiyo.
Taarifa ya FA ilieleza kuwa Man City walishindwa kuwazuia wachezaji wao kujihusisha na tabia ambazo si sahihi uwanjani na wametakiwa hadi Desemba 7 wawe wamejibu tuhuma hizo.
Hooper hata hivyo alionekana kujichanganya baada ya kuruhusu mchezo uendelee kwa kuwapa Man City ‘advantage’ lakini ghafla aliamuru City wapewe mpira wa adhabu wakati wachezaji wake walikuwa wakielekea kuliona lango la Tottenham.
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland ndiye aliyekuwa mstari wa mbele pamoja na wachezaji wenzake kwa kumzonga Hooper na baada ya hapo alitumia mtandao wa Twitter (sasa X) kumsakama mwamuzi huyo.
Taarifa ya FA hata hivyo haikueleza kama Haaland atapewa adhabu tofauti peke yake kwa kosa la kumshambulia mwamuzi huyo kwenye mtandao wa X.
Kimataifa Man City hatiani kwa kumzonga mwamuzi
Man City hatiani kwa kumzonga mwamuzi
Read also
