Na mwandishi wetu
Bao la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua dhidi ya Al Ahly limechaguliwa kuwa bao bora la wiki la mechi za raundi ya pili hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mtandao rasmi wa michuano hiyo uliweka video ya bao la Pacome na kuandika: “Ndani ya Tanzania, katikati ya mabeki watatu, bao bora la wiki la mechi za pili limekwenda kwa Pacome Zouzoua wa Yanga.”
Kiungo huyo alifunga bao hilo kwa shuti kali ndani ya 18 akiwa amezungukwa na msitu wa mabeki wa Al Ahly kwenye dakika za lala salama katika mchezo huo uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Bao hilo lilipindua matokeo na kuwa sare ya 1-1 na hivyo kuinusuru timu hiyo na kipigo cha pili mfululizo katika mechi za Kundi D baada ya awali kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad.
Mbali na kufunga bao hilo, kiungo huyo raia wa Ivory Coast alionesha uwezo mkubwa ikiwemo kutengeneza nafasi kadhaa ambazo wenzake walishindwa kuzitumia ipasavyo.
Pacome aloyejiunga na Yanga msimu huu akitokea ASEC Mimosas, anaungana na Mudathir Yahya na Fiston Mayele ambao mabao waliyoifungia timu hiyo msimu uliopita kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika yalishinda tuzo za mabao bora ya wiki.
Kimataifa Bao la Pacome lang’ara Afrika
Bao la Pacome lang’ara Afrika
Read also
