Nantes, Ufaransa
Klabu ya Ufaransa imesema kwamba mmoja wa mashabiki wake ameuawa baada ya kushambuliwa katika tukio lililotokea jana Jumamosi kabla ya mechi yao na Nice.
Taarifa ya Nantes ilieleza kwamba shabiki huyo aliumizwa vibaya na kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari shabiki huyo ni mwanachama wa moja ya makundi ya mashabiki wakereketwa wa klabu hiyo.
“Katika tukio ambalo tayari linafanyiwa uchunguzi na vyombo vya usalama, shabiki huyo mwenye umri wa miaka 31 alizimia baada ya kupigwa kwa nyuma,” ilieleza taarifa ya klabu ya Nantes.
Kwa mujibu wa klabu hiyo licha ya watu wa huduma ya kwanza kuwahi kutoa msaada lakini ilibainika kwamba isingewezekana kuokoa maisha ya shabiki huyo.
Gazeti la L’Equipe la nchini Ufaransa katika taarifa yake lilieleza kuwa tukio hilo lilianza baada ya magari yaliyokuwa na mashabiki wa timu ya Nice kuvamiwa na makundi ya mashabiki pinzani.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1, Nantes licha ya kujikuta katika majonzi ya kumpoteza shabiki wao lakini ilitoka na ushindi wa bao 1-0.
