Na mwandishi wetu
Baada ya Mtibwa Sugar kupoteza mchezo wa nne mfululizo wa Ligi Kuu NBC, kocha wa timu hiyo, Zuberi Katwila amesema wanahitaji kufanya kazi kubwa kuboresha safu ya ulinzi ili mambo yaende sawa.
Akizungumza baada ya mechi waliyopoteza jana kwa mabao 2-1 dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Katwila alisema hazungumzi hayo kwa ajili ya kulaumu isipokuwa kama makocha wamezibeba kasoro hizo na wanakwenda kuzifanyia marekebisho.
“Soka ndio lilivyo wakati mwingine lakini kufungwa sio kuzuri, haina mwendelezo mzuri kwetu, ila sasa tuna kazi kubwa ya kufanya ili kutengeneza ulinzi mzuri, tusifungwe tupate uwiano mzuri na hii sio sehemu ya kulaumiana ila kama makocha tumeliona hilo na kazi yetu ni kurekebisha,” alisema Katwila.
Alisema pamoja na kupoteza mechi hiyo lakini pia kuna mabadiliko ameyaona ndani ya kikosi yanayoleta mwanga mzuri, akiamini watakaa sawa muda si mrefu na wataondokana na presha ya kupoteza waliyonayo sasa.
Naye Kocha Mkuu wa Tabora, Goran Kopunovic alisema: “Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza lakini cha pili hatukucheza vizuri, hilo nitalifanyia kazi ila nawapongeza wachezaji wangu, muhimu pointi tatu tumezipata na hii inatupa nguvu ya kujiamini na kupambana zaidi.”
Mtibwa inaburuza mkia ikiwa na pointi tano baada ya mechi 11, ikishinda moja, sare mbili na kufungwa mara nane. Tabora ipo nafasi ya nane kwa pointi 14 baada ya mechi 10, ikishinda mechi tatu, sare tano na imefungwa mara mbili.
