Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa zamani wa Simba SC, Aden Rage amempongeza Rais wa Yanga, Hersi Said kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Afrika (ACA).
Rage baada ya pongezi hizo pia alisema kwamba klabu za Tanzania sasa zitafaidika mno na wadhifa wake huo mpya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumamosi, Rage alisema kwa namna anavyomfahamu Hersi ni imani yake kwamba klabu za Tanzania bila kujali upinzani uliopo, zote zitafaidika na uwepo wa Hersi kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
“Kwanza nimpongeze Injinia Hersi kwa kuchaguliwa kwa kishindo sababu kura zilikuwa 15, yeye akapata tisa kwa hiyo ni ushindi wa kujivunia na ni rekodi katika historia ya Tanzania.
“Bahati mbaya Watanzania wengi tunashindwa kufahamu kwamba unapopata Mtanzania anayeingia kwenye hizi taasisi za kimataifa kama Caf na Fifa unatakiwa ushukuru kwa kuwa ni bahati kwetu, nina imani ninavyomjua Hersi bila Yanga, Simba, Azam au klabu nyingine yoyote tutafaidika sana na uwepo wake mule,” alisema Rage.
Rage alisema kwa kuwa wadhifa huo unamfanya Hersi kuingia katika Kamati ya Utendaji ya Caf basi itakuwa rahisi kuwakilisha pia matatizo ya timu za ndani ya nchi yake na klabu zote Afrika zitafaidika kwa uwepo wa ACA.
Hersi alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho juzi katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Marriot Mena House mjini Cairo, Misri pamoja na manaibu wake wawili; Jessica Mataung wa Kaizer Chiefs na Paul Basset wa Akwa United.
