Na mwandishi wetu
Tanzania imeendelea kusalia kwenye nafasi ya 121 katika viwango vya ubora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa mwezi Novemba.
Katika mwezi huo, Tanzania ilicheza michezo miwili ya kimataifa ambapo ilishinda dhidi ya Niger kwa bao 1-0 kabla ya kufungwa na Morocco mabao 2-0, zote zikiwa ni mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa mtandao rasmi wa Fifa uliotoa viwango hivyo vipya, Tanzania imeendelea kusalia katika nafasi hiyo iliyoishikilia tangu mwezi Oktoba, mwaka huu mara ya mwisho kutolewa viwango hivyo vya Fifa.
Kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Jamhuri ya Kidemokdasi ya Congo ni ya 67 ikishuka nafasi mbili, Uganda imeshika nafasi ya 92 nayo pia ikiendelea kuporomoka kwa nafasi mbili wakati Kenya iking’ang’ana katika nafasi ya 110.
Sudan yenyewe imepanda mpaka namba 128 kutoka nafasi ya 130, Rwanda imetoka nafasi ya 140 mpaka 133 na Burundi imetoka namba 142 na kushika namba 139 huku Ethiopia ikishuka kwa nafasi moja ikiangukia nafasi ya 144 na Sudan Kusini ni ya 166 ikipanda kwa nafasi moja.
Kwa Afrika, Morocco imeendelea kuwa kinara ikishika nafasi ya 13 ikifuatiwa na Senegal nafasi ya 20, Tunisia ikipanda mpaka namba 28 kutoka namba 32, Algeria ya 30, Misri ya 33, Nigeria ya 42 wakati Cameroon ya 46 na Ivory Coast ni ya 50.
Kidunia, Argentina inashika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Ufaransa na England imeshika nafasi ya tatu na kuitoa Brazil ambayo imeangukia nafasi ya tano. Ubelgiji ni ya nne na Uholanzi ni ya sita ikifuatiwa na, Ureno, Hispania, Italia na Croatia inayohitimisha 10 bora.
Kimataifa Tanzania yashindwa kupanda Fifa
Tanzania yashindwa kupanda Fifa
Read also
