Na mwandishi wetu
Droo ya hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) au Kombe la FA, imechezeshwa Dar es Salaam Jumatano hii ambapo vigogo Yanga wataanza na Haulung wakati mahasimu wao Simba wataikabili Tembo ya Nzega.
Jumla ya timu 64 zikiwemo za Ligi Kuu NBC zimehusika katika upangwaji wa droo hiyo kuelekea hatua inayofuata ya 32 bora ya michuano hiyo.
Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo wamepangwa kuanza na Haulung ambayo ni timu ya daraja la kwanza wakati watani zao Simba wakipangwa na Tembo FC ya Nzega na Azam ikipangwa kukutana na Alliance ya Mwanza.
Meneja wa Mashindano wa TFF, Baraka Kizuguto alisema mechi za awali za michuano hiyo zitaanza kuchezwa kuanzia Desemba 15 hadi 17, mwaka huu.
Kizuguto alisema maandalizi yote kuelekea mechi hizo yanakwenda vizuri na wanatarajia kuwa na mashindano bora kutokana na kuimarika kwa baadhi ya mambo ukilinganisha na mwanzoni wakati mashindano hayo yanaanza.
“Wito wangu kwa klabu shiriki ni kufanya maandalizi ili kutoa upinzani sababu hii ni fursa pekee hasa kwa timu za madaraja ya chini kama zitafanya vizuri na kufika hatua za juu ikiwemo ubingwa zinaweza kuwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa,” alisema Kizuguto.
Klabu za Simba na Yanga ndio zinaongoza kulibeba taji hilo ambapo kila mmoja ametwaa kombe hilo mara tatu wakifuatiwa na Azam FC iliyolibeba mara moja sawa na Mtibwa Sugar.
