Na mwandishi wetu
Bondia Hassan Mwakinyo ‘Champez’ ameeleza furaha yake na kuishukuru serikali kupitia Wizara ya Utamaduni na Michezo kwa kulimaliza suala lake na kuondolewa adhabu ya kufungiwa kutoshiriki mchezo huo kwa mwaka mmoja na faini ya Sh milioni moja.
Mwakinyo amezungumza hayo na GreenSports leo Jumanne baada ya jana Jumatatu Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kumuondolea kifungo hicho walichomwadhibu Oktoba 10 mwaka huu.
Bondia huyo aliadhibitiwa baada ya kutopanda ulingoni kuzichapa na Julius Indongo wa Namibia Septemba 29, mwaka huu akidai mapromota walikwenda kinyume na makubaliano yao.
“Kwanza namshukuru Mungu maana nilikuwa na imani ya kutokaa muda wote huo bila kupigana na mwisho amesikia ndoto yangu na pia BMT (Baraza la Michezo Tanzania) kupitia Wizara wamelisimamia hili na kulimaliza vizuri kwa faida ya michezo Tanzania.
“Nafikiri ilionekana haja ya kumaliza hili ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo hapa nchini na nashukuru baada ya vikao vya maridhiano ya pande zote mbili, tumefanikiwa kulimaliza na sasa nipo huru,” alisema Mwakinyo.
Bondia huyo pia amewaeleza mashabiki wake kuwa anafahamu jinsi gani wanatamani kumuona akipigana kama yeye anavyotamani kupanda ulingoni kwa ajili yao.
Mwakinyo aliwataka mashabiki hao wakae tayari kwani kuna mazungumzo yanaendelea na pengine Desemba, mwaka huu anaweza kuwa na pambano la kufungia mwaka 2023.
