Na mwandishi wetu
Kocha mpya wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amesema anafahamu alichokuja kukifanya Simba na si kingine zaidi ya kuipa mafanikio na kuwafurahisha mashabiki timu hiyo kila wakati.
Benchikha raia wa Algeria ameyasema hayo muda mfupi baada ya kutua nchini usiku wa kuamkia leo Jumanne sanjari na kocha msaidizi, Fardi Zemiti na kocha wa viungo, Kamal Boudjenane.
Kocha huyo ametua ikiwa ni siku nne tangu atangazwe rasmi kujiunga na Wekundu hao kurithi mikoba ya Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ huku Boudjenane akitua kuziba nafasi ya Hategekimana Corneille aliyetimuliwa siku moja na Robertinho baada ya timu hiyo kufungwa mabao 5-1 na Yanga wiki tatu zilizopita.
“Nafahamu kilichonileta hapa, nipo hapa kwa ajili ya kushinda, kwa ajili ya mafanikio, tuko hapa kwa ajili ya Simba na kwa ajili ya mashabiki wote wa Simba, tunapaswa kuwa imara zaidi kwa ajili ya kuonesha kiwango kizuri uwanjani pia.
“Najua namna wanavyofikiri (mashabiki) kuhusu mimi, nafahamu yoye hayo na inaonesha napaswa kuwa imara ili kuwapa furaha mashabiki maana bila wao Simba haina kitu, tunatakiwa kupambana na kuonesha kiwango kuwapa furaha mashabiki,” alisema Benchikha.
Benchikha aliyeondoka USM Alger baada ya kuwapa taji la Shirikisho Afrika msimu uliopita na ndoo ya CAF Super Cup ‘alipoinyoosha’ Al Ahly mwanzoni mwa msimu huu, kibarua chake cha kwanza kwa Lunyasi kitakuwa dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Simba itashuka Uwanja wa Obed Chilume, Francistown, Desemba 2, mwaka huu kwa ajili ya mchezo huo wa pili wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya 1-1 na ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Simba inahitaji ushindi huo wa kwanza kupunguza machungu ya kukosa ushindi kwenye mechi zake tatu mfululizo zilizopita ambapo ukiachana na kipigo cha Yanga, kabla ya sare ya ASEC pia timu hiyo ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu NBC.
