London England
Kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya England, Terry Venables (pichani) amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Venables anakumbukwa kwa kuinoa England kati ya mwaka 1994 hadi 1996 lakini zaidi anakumbukwa kwa kuifikisha timu hiyo hatua ya nusu fainali ya Euro 96, fainali ambazo zilifanyika England.
Kabla ya kuwa kocha, Venables alizichezea Chelsea, Tottenham na Queens Park Rangers kabla ya kuwa kocha ambapo mbali na timu ya England pia amewahi kuzinoa timu za Barcelona na Tottenham.
“Tumeumizwa mno kwa kumpoteza mume wa aina yake na baba ambaye amefariki dunia kwa amani jana (juzi) baada ya kuugua kwa muda mrefu,” ilieleza taarifa ya familia ya kocha huyo.
“Tungeomba tuendelee na taratibu za kifamilia katika kipindi hiki cha huzuni ili kuturuhusu kuomboleza kifo cha mtu huyu mpendwa ambaye tunajiona wenye bahati kuwa naye katika maisha yetu,” ilifafanua taarifa ya familia.
Akiwa kocha mbali na kuifikisha England nusu fainali ya Euro 96, Venables pia aliwahi kutwaa taji la La Liga na Barcelona na kuifikisha timu hiyo katika hatua ya fainali Ulaya na akiwa na Tottenham alibeba Kombe la FA.
Enzi zake akiwa mchezaji, Venables alicheza mechi zaidi ya 500 katika klabu za Queens Park Rangers, Tottenham na Chelsea wakati timu ya England aliwahi kuichezea mara mbili tu.
Nahodha wa zamani wa England, Gary Lineker, akimzungumzia kocha huyo alisema, “hakuwa tu kocha bali pia alikuwa rafiki, mchangamfu, mzungumzaji lakini pia alikuwa mkali, na hivyo ndivyo unavyotakiwa uwe, alilielewa soka, alikuwa kichwa cha soka.”
Nahodha mwingine wa England, Alan Shearer ambaye alikuwamo katika kikosi cha England kwenye Euro 96, alisema, “hakika ni habari ya kusikitisha, shujaa Terry Venables ameaga dunia, Pumzika kwa Amani bosi, ulikuwa mtu wa kipekee, nina deni kubwa kwako.”
